JOHN OBI MIKEL AAGA CHELSEA KWENDA CHINA, MARCO SILVA BOSI MPYA HULL CITY!

MNIGERIA John Obi Mikel ametangaza kuihama Chelsea kujiunga na Klabu ya China Tianjin TEDA wakati Hull City ikitangaza kumteua Bosi wa zamani wa Olympiakos na Sporting Lisbon kuwa Meneja wao Mpya.

JOHN OBI MIKEL AIGA CHELSEA KWENDA CHINA

JOHN-OBI-MIKEL-CHINAJohn Obi Mikel ametangaza kupitia Posti kwenye Mitandao ya Kijamii kuihama Chelsea kujiunga na Klabu ya China inayocheza Supa Ligi Tianjin TEDA.

Mikel, mwenye Miaka 29, alijiunga na Chelsea akiwa na Miaka 19 akitokea Klabu ya Norway Lyn Mwaka 2006 na kucheza Mechi 374.

Lakini Msimu huu, chini ya Meneja Mpya Antonio Conte, Mikel hajacheza hata Mechi moja na hilo limemfanya ahame.

Akiwa na Chelsea, Mikel alitwaa Makombe 11 yakiwemo Mawili ya Ubingwa Ligi Kuu England na moja la UEFA CHAMPIONZ LIGI.

Akiaga, Mikel alitoa Shukran kwa Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich pamoja na Mashabiki wa Klabu hiyo.

MARCO SILVA BOSI MPYA HULL CITY!HULL-SILVA

Marco Silva, Raia wa Miaka 39 kutoka Ureno, ameteuliwa kuwa Meneja Mpya wa Hull City kuchukua nafasi ya Mike Phelan ambae alitimuliwa Jumanne iliyopita kufuatia matokeo mabovu yaliyoiacha Klabu hiyo ikiwa mkiani mwa EPL, Ligi Kuu England.

Hull City wapo Nafasi ya 20, ya mwisho kabisa, wakiwa Pointi 3 nyuma ya Timu ya 17 ambayo ndio nafasi salama kwenye EPL.

Silva alieanza Ukocha Mwaka 2011 akiwa na Klabu ya Daraja la Pili Estoril na kuipandisha Daraja na kisha Mwaka 2014 kuhamia Sporting Lisbon huko Ureno ambako aliiwezesha kutwaa Kombe la Ureno lakini akatimuliwa Juni 2015 ikiwa ni Siku 4 tu baada ya kutwaa Kombe hilo kwa madai ya kutovaa Sutu rasmi ya Klabu kwenye mojawapo ya Mechi zao.

Mwezi Julai 2015, Silva akajiunga na Klabu ya Ugiriki na kuiwezesha kucheza Mechi 17 za ushindi mfululizo na pia kuitwanga Arsenal 3-2 Uwanjani Emirates, London kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI.

Baada ya kuipa Ubingwa wa Ugiriki, Silva akaamua kuondoka Olympiacos mwishoni mwa Msimu uliopita na tangu wakati huo alikuwa hana kibarua.