NINGEKUWA GEORGE LWANDAMINA…

Na Mwandishi Wetu

received 1116887348410041MOJA kati ya burudani kubwa watakayokutana nayo Wazanzibari kwa mwaka 2017, ni kuutazama mchezo wa kwanza wa ‘Dar es Salaam derby’ ukichezwa katika ardhi yao.
Simba watavaana na Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, ni mchezo wa kikubwa unaohitaji maamuzi ya kikubwa kuuamua.
Mimi ningekuwa kwenye nafasi ya kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ningefanya mabadiliko kwenye mambo matatu makubwa ambayo kwa namna moja au nyingine yangeweza kuisaidia Yanga kupata ushindi dhidi ya Simba na kufuta aibu ya kichapo cha bao 4-0 walichokipata mbele ya Azam.
Kwanini Makapu na si Zulu?
Katika michezo michache aliyocheza akiwa na jezi ya Yanga, tayari Justine Zulu ameshaonyesha ni mchezaji wa aina gani.
Ni mtulivu, mbunifu asiye na haraka uwanjani. Anakaba kwenye njia, si kiungo wa kukaba mtu kwa mtu, kitaalamu inaitwa ‘man to man marking’.
Kwa aina yake ya uchezaji si mtu sahihi sana kwenye safu ya kiungo ya Yanga kwenye mchezo dhidi ya Simba. Kwanini? Ipo sababu moja tu ya msingi.
Dakika 90 za pambano la Azam zimetosha kabisa kuuonyesha udhaifu wa Zulu pindi anapokutana na viungo wasumbufu na wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.
Kuzidiwa kwa safu ya kiungo, kuliifanya safu ya ulinzi iliyokuwa ikiongozwa na Dante na Yondani kuelemewa na mashambulizi na wakati mwingine kupelekea kufanya makosa mengi yalioigharimu Yanga.
Uwepo wa Makapu utapunguza muda wa viungo wa Simba kukaa na mpira na kutengeneza nafasi, ni hatari zaidi kama utamwachia Muzamir sekunde tano za kukaa na mpira huku akilitazama lango lako.
Yanga wanamhitaji zaidi Makapu kuilinda safu yao ya ulinzi kwa kumnyima uhuru Muzamir, Zulu asubiri kwanza!
Kwanini Kaseke na si Msuva?
Unaweza ukawa umeshtuka hapa, lakini haya ndiyo mabadiliko ambayo ningeyafanya katika kikosi cha Yanga, kwanini Msuva hastahili kuanza kwenye pambano hili?
Kwanza Lwandamina anatakiwa afahamu presha waliyonayo Yanga kwenye pambano hili, ushindi dhidi ya Simba ni muhimu zaidi ya Kombe la Mapinduzi.
Ili kuikwepa presha ya mchezo huu unatakiwa kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuhimili presha ya matokeo, rekodi ya Msuva dhidi ya Simba inafahamika.
Kwa faida yake na timu, Msuva si mtu sahihi kwa kuanza pambano hili. Hii ni sababu ya kwanza, ya pili ipo kiufundi zaidi.
Ni kama Yanga wameshazoeleka kimfumo na ni rahisi mno kupambana nao kwa kuwa kila kocha anajua kuwa uimara wao uko kwenye wingi za pembeni.
Unaweza kuwavuruga Simba kwa kumweka nje Msuva na kumpanga Kaseke ukiwa na mbinu nyingine ya kimchezo, mbinu gani? Tulia nikwambie.
Kwa kuitazama Simba, uimara wao umejengwa kupitia wachezaji wawili kwenye safu yao ya kiungo. Jonas Mkude na Muzamir Yassin.
Mkude ndiye anayetengeneza mashambulizi ya Simba kutoka nyuma na Muzamir ndiye anayemaliza kazi kwa kupiga asisti ya mwisho au kufunga, unahitaji kuwa na wachezaji wawili kuwapoteza watu hawa.
Muzamir tayari atakuwa kazini na Makapu na si mbaya ukampanga Kaseke kudili na Jonas Mkude, kuna faida inaweza kupatikana hapa, kivipi? Mfumo wangu utaeleza zaidi.
Kwanini 4-2-3-1?
Golini bado ningemweka Deogratius Munishi ‘Dida’, watu wanne wa nyuma ningeweka wale wale, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Dante na Kelvin Yondani.
Viungo wawili wa kati, ningewapanga Makapu na Deus Kaseke, watatu wa mbele kidogo ningewasimamisha Haruna Niyonzima (akicheza kutoka upande wa kulia), Kamusoko na Donald Ngoma (akishambulia kutoka kushoto), mbele angesimama Amissi Tambwe.
Nini nategemea kwenye mfumo huu? Kwanza Lwandamina anatakiwa aamini kuwa Kamusoko si mkabaji, ni kiungo mchezeshaji anayetakiwa kuwa huru katikati ya uwanja.
Ukimpanga pamoja na Haruna ni lazima uhakikishe una watu wawili wenye mapafu ya mbwa kuusaka mpira, hapa ndipo ninapoiona faida ya Kaseke kwenye mfumo huu.
Kazi ya Kaseke ni kuhakikisha Mkude hapati nafasi ya kutulia na mpira na Makapu kazi yake ni kumpoteza Muzamir dimbani.
Ukimpoteza Mkude na Muzamir na ukamuweka Ngoma upande wa kushoto, ni wazi utaiua nguvu ya Simba katikati na upande wa kulia.
Omog amekuwa na tabia ya kumpanga Shiza Kichuya upande wa kulia, faida ya Kichuya ipo pale timu inaposhambulia lakini si mtu mwenye uwezo wa kushuka na kumsaidia Bukungu.
Ngoma akicheza kutoka kushoto, bila shaka utaua safari za Bukungu na utamfanya Abdi Banda kutumia muda mwingi pembeni ya uwanja.
Banda akisogea kushoto ni faida kwa Tambwe atakayesalia katikati na Method Mwanjali. 
Upande wa kushoto, Niyonzima atakuwa na Tshabalala. 
Unaijua faida ya Niyonzima upande huo? Kumzidi Tshabalala hutakiwi kuwa na mbio, asilimia 90 ya uchezaji wao inatakiwa iwe akili na nguvu.
Niyonzima atamfanya Tshabalala awe naye kwa makini zaidi na kutoa mwanya kwa Juma Abdul kucheza kwa urahisi na winga wa Simba, yoyote yule atakayepangwa, iwe Mo Ibrahim au Pastory Athanas, wote ni watu ambao Juma ana uwezo wa kucheza nao ‘one against one situation.’