WENGER ‘APOZA’ HASIRA ZA ALEXIS SANCHEZ, ATOBOA UPUNGUFU KIUNGO!

WENGER-SANCHEZMENEJA wa Arsenal Arsene Wenger amezipuuza ripoti kuwa Alexis Sanchez yu tayari kuihama Klabu hiyo baada ya Jumanne Usiku kuonyesha hasira kwenye Mechi na Bournemouth.

Baada ya Mechi hiyo kwisha Sanchez alitupa Glovu zake chini na kugoma kujumuika na wenzake kusherehekea Sare ya 3-3 waliyoipata baada kutoka nyuma 3-0.

Pia iliripotiwa Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Chile pia alikaa kimya kwenye Chumba cha Kubadili Jezi lakini Wenger amepuuzia taarifa hizo na kudai ni kawaida kutokuwa na furaha usiposhinda Mechi.

Vile vile Wenger alifafanua kuhusu maendeleo ya Majeruhi wao Viungo wao Cazorla, Coquelin na Ozil,

Hivi sasa Arsenal wana uhaba mkubwa kwenye Kiungo kufuatia kuumia kwa Francis Coquelin, ambae atakuwa nje kwa Wiki 4, na Santi Cazorla kuchelewa kupona maumivu yake huku Mo Elneny akijiunga na Timu ya Taifa ya Egypt kwa ajili ya AFCON 2017, Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Pengo hili litaifanya Arsenal kuwatumia Granit Xhaka na Aaron Ramsey pekee kwenye Kiungo, upacha ambao ulipwaya mno kwenye Mechi na Bournemouth,

Wenger ameeleza: “Coquelin yupo nje kwa Wiki 3 au 4 akisumbuliwa na Musuli za Pajani. Uponaji wa Cazorla unachelewa!”

Nae Kiungo mwingine Mesut Ozil ni Mgonjwa akiwa na tatizo la Koo.

Vile vile, Wenger alitoboa kuwa kwenye Mechi yao ya Raundi ya 3 ya FA CUP ambayo wataivaa Preston Ugenini hapo Jumamosi, Alexis Sanchez, Lauremt Koscielny na Petr Cech, watapumzishwa.

Kuhusu Straika Danny Welbeck, ambae ameanza Mazoezi baada ya kupona Goti ambalo limemweka nje kwa Miezi kadhaa, Wenger ameeleza hajaamua kama acheze Mechi na Preston.